Rais Kim Jong Un wa Korea Kaskazini amesema nchi za Marekani na Korea Kusini zinahatarisha usalama, hivyo mpango wa silaha wa nchi hiyo yakiwemo makombora ya masafa marefu unalenga kukabiliana na kitisho cha nchi hizo.
Rais Kim Jong Un ametoa kauli hiyo mjini Pyongyang, wakati wa zoezi la kukagua silaha kadhaa yakiwemo makombora ya masafa marefu.
Korea Kaskazini na Korea Kusini ambazo ni majirani, zimekuwa katika mvutano wa muda mrefu ambao unahusisha kutoleana vitisho ikiwa ni pamoja na kuonyesha uwezo wa nguvu za kijeshi.
Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Korea Kusini, imekuwa ikiendesha mazoezi ya pamoja ya kijeshi yakilenga kuitisha Korea Kaskazini, ambayo nayo mara kadhaa imekuwa ikifanya majaribio ya kurusha makombora ya masafa marefu ikizitisha Korea Kusini na Japan ambazo ni washirika wa Marekani.
Wiki mbili zilizopita Korea Kusini na ile ya Kaskazini zilirejesha mawasiliano ya simu ya moja kwa moja, ikiwa ni ishara ya kupunguza uhasama kati yao.