Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika jana nchini Urusi yanaonesha Vladimir Putin anayeshikilia kiti hicho kwa sasa anaongoza.
Kwa mujibu ya matokeo hayo ya awali, Putin amepata asilimia 87.8 ya kura zote zilizopigwa, ikiwa ni matokeo ya juu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Urusi baada ya muungano wa Kisovieti kuvunjika.
Matokeo hayo yanampa ushindi wa kishindo Putin mwenye umri wa miaka 71.
Hiki kitakuwa ni kipindi chake cha tano na hivyo kumfanya ampiku Josef Stalin na kuwa kiongozi wa muda mrefu zaidi wa nchi hiyo kuwahi kutokea kwa zaidi ya miaka 200.
Mataifa mbalimbali yakiwemo Marekani, Ujerumani na Uingereza yamesema uchaguzi huo haukuwa huru na haki kutokana na kufungwa kwa wanasiasa wa upinzani na wengine kudhibitiwa.