PSSSF yatakiwa kuongeza makusanyo

0
582

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Menejimenti ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutafuta mbinu mpya za kuongeza makusanyo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipokutana na menejimenti ya mfuko huo baada ya kutembelea ofisi za PSSSF kwa lengo la kufahamiana na Menejimenti hiyo.

Amesema kuwa amepokea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu na kubaini kuwa ukusanyaji wa michango hauridhishi.

“Mfuko huu ni wa tofauti na wa NSSF kwa sababu umeunganisha mifuko mingine ya GEPF, PSPF, LAPF na PPF, Mifuko yote hii ilikuwa na malengo na majukumu yake ya awali, lakini sasa imeunganishwa kwa hiyo jukumu letu ni moja,” amesema Waziri Mkuu.

Ameitaka menejimenti hiyo pia ijiridhishe juu ya uhakiki wa mali walizorithi kutoka mifuko mingine na izitambue ziko katika hali gani.

“Menejimenti peke yenu hamuwezi kufuatilia mali zote, kwa hiyo wapeni hiyo kazi wajumbe wa Bodi, wagawane maeneo ili waende kuzitathmini hizo mali na kisha nipate hiyo taarifa,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa mfuko huo kuanzia Agosti Mosi mwaka 2018 hadi Machi 31 mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, -Hosea Kashimba alisema kuwa majukumu makubwa ya mfuko huo ni kusajili wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa wanachama.