Profesa Kikula aipongeza kurugenzi ya ukaguzi migodini

0
230

Mwenyekiti wa tume ya madini Profesa Idris Kikula, amepongeza kazi nzuri ya uelimishaji wa wachimbaji wadogo wa madini inayofanywa na kurugenzi ya ukaguzi wa migodi na mazingira ya tume ya madini nchini.

Profesa Kikula ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Novemba, 2020 kwenye mafunzo ya wachimbaji wadogo, wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika mikoa ya kimadini ya Mbeya, Chunya na Songwe yenye lengo la kuwapa uelewa mpana kuhusu masuala ya usalama, afya, utunzaji wa mazingira, usafirishaji na matumizi sahihi ya baruti kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

Amesema kuwa, elimu ambayo inatolewa na wataalam wa tume ya madini lengo lake ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wanachimba madini yao na kupata faida kubwa, huku wakizingatia masuala ya afya na mazingira ili kuepusha ajali na kusisitiza kuwa, elimu imeshatolewa katika mikoa ya Singida, Katavi na Manyara na itaendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini.

“Nampongeza Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga, mameneja wake na wataalam kwa utaratibu mzuri waliouweka wa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini, rai yangu waendelee na utaratibu huu katika mikoa ya kimadini mingine yote.”- amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Prof. Kikula amewataka wachimbaji wa madini kutumia Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), kuwasilisha kero zao na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kutatua changamoto zote.