Profesa Kanywanyi kuzikwa Dar es salaam kesho

0
200

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam umeelezea kusikitishwa na kifo cha Profesa wake nguli wa sheria Josephat Kanywanyi kilichotokea Januari 10 mwaka huu nyumbani kwake jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na chuo hicho imeeleza kuwa, mwili wa Profesa Kanywanyi aliyewahi kuwa Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria kwa muda mrefu zaidi,  utaagwa na kuzikwa kesho katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es salaam.

Profesa Kanywanyi aliyezaliwa Novemba 5 mwaka 1933 huko Bukoba mkoani Kagera,  ni mmoja wa Watumishi waliofanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa muda mrefu.

Alijiunga na  Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki  mwaka 1963 na kuhitimu shahada ya kwanza ya sheria mwaka 1966.

Mwaka 1967 alihitimu Shahada  ya Uzamili ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Califonia nchini Marekani,  na  mwaka 1987 alihitimu shahada ya uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Kanywanyi ameshika nafasi mbalimbali katika kilichokuwa kitivo cha Sheria na sasa Shule Kuu ya Sheria ikiwa ni pamoja na kuongoza kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 1974 mpaka 1979 na mwaka 1982 mpaka 1985 akiwa ndiye Profesa  aliyeongoza shule ya sheria kwa muda mrefu zaidi.

Mwezi Julai mwaka 2020 Profesa Kanywanyi aliteuliwa kuwa Profesa Emeritus,  nafasi ambayo amedumu nayo hadi umauti ulipomkuta.

Profesa Kanywanyi ataagwa rasmi na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam hapo kesho katika ukumbi wa Nkurumah.