Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema nyakati za kubembelezana katika kazi zimepitwa na wakati.
Profesa Ndalichako amesema hayo mkoani Dar es Salaam, wakati akizindua Baraza la Saba la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), lenye jukumu la kuchapisha na kuidhinisha machapisho ya vitabu mbalimbali vya elimu na kusambazwa kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu nchini.
“Zama za kubembeleza watu kufanya kazi zimepitwa na wakati, fanyeni kazi kwa weledi kwa maslahi ya Wananchi kwa ujumla, na mtu akionekana hatoshi atafutwe mwingine ili twende na kasi ya Serikali,” amesema Profesa Ndalichako
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutatua changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya kuiwezesha kusimamia elimu nchini.
Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1. 47 ili kufanya mapitio ya mitaala kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu na shilingi bilioni 15.5 zimetolewa kwa ajili ya uchapishaji wa vitabu vya sekondari.