Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa hali ya upatikanaji wa saruji nchini ni ya kuridhisha na viwanda vya saruji kwa sasa vinatoshereza mahitaji ya nchi.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo Oktoba 15, 2021 alipotembelea kiwanda cha Saruji cha Twiga ili kujiridhisha na uzalishajii na upatikanaji wa saruji baada ya Tanzania kunufaika fedha za mkopo wa Shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani zitatumika katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za jamii katika sekta ya Afya, Elimu, Utalii na Maji.
“Niwahakikishie Watanzania hali ya upatikanaji wa saruji nchini ni mzuri kulingana na mahitaji ya saruji na viwanda tulivyonavyo hakuna changamoto,” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo
Amesema hali ya umeme katika viwanda inaendelea kuboreka lakini bado kuna changamoto kidogo ambazo atakutana wa Waziri wa Nishati, January Makamba ili kuhakikisha changamoto ya umeme katika kiwanda cha Twiga na viwanda vingine nchini inakwisha kabisa.
Aidha, Prof. Mkumbo amekutana na kufanya mazungumzo na mjumbe wa kampuni iliyowekeza katika kiwanda hicho kutoka Ujerumani ili kujadili maendeleo ya kiwanda na kumpa uhakika kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wao ambao wamefanya na wanaendelea kupanua.