Polisi wakamata mashine 153 za Kamari

0
302

Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Maafisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha wamewakamata watu Watano na mashine 153 za Kamari ambazo zimeingizwa nchini kinyume na taratibu.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema mashine hizo zimekamatwa katika operesheni iliyofanyika kuanzia Julai 05, 2023 na kukamilika Julai 07, 2023.

Amesema mkoa wa Kilimanjaro hautafumbia macho mashine za aina hiyo kuingizwa kinyume cha taratibu kwani zimekuwa zikitumika isivyo halali ikiwemo baadhi ya Wanafunzi kujihusisha na michezo ya Kamari.

Kwa upande wake Meneja Ukaguzi na Udhibiti kutoka Bodi ya Michezo ya kubahatisha nchini Sadiki Eliusu amesema wamekagua mashine hizo zote na kubaini hazina usajili wa bodi jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji

Eliusu ameongeza kuwa mashine hizo zikiwa wa usajili zinasaidia mapato ya Serikali kukusanywa kwa urahisi na kwamba kwa sasa kitakachofanyika ni kuziteketeza.