Polisi Tanga wapiga marufuku Disko toto wakati wa Krismasi na mwaka mpya

0
191

Jeshi la Polisi mkoani Tanga limepiga marufuku madisko toto wakati wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kutokana na kwamba baadhi waendeshaji wake kutokuwa waangalifu na kuingiza idadi kubwa ya watoto kuliko uwezo wa maeneo husika.

Marufuku hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga Blasius Chatanda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna walivyojipanga kuimarisha ulinzi wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ambapo amesema wameamua kupiga marufuku madisko toto kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza.

Kamanda Chatanda amesema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na tabia ya baadhi ya wanaofanya shughuli hizo kutokuwa waangalifu kwenye dadi ya watoto wanaoingia kwenye madisko toto na hivyo kuhatarisha maisha ya watoto.

“Tumepiga marufuku aina yoyote ya madisko toto katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya kutokana na baadhi ya waendeshaji wake kutokuwa waangalifu na kupelekea kuingiza idadi kubwa ya watu, hali inayosababisha kukosekana kwa hewa na wakati mwingine kukanyagana,”amesema Kamanda Chatanda.

“Lakini pia nishauri wenye maeneo ya kumbi za stahere wawe na tahadhari ya ulinzi wa ndani kwa sababu hawawezi kujua walioingia wana nia gani, hivyo wahakikishe wanakuwa makini kwa lengo la kuepusha kutokea matukio ambayo yanasababisha uvunjifu wa amani kwenye maeneo yao” ameshauri Kamanda huyo wa polisi wa mkoa wa Tanga.

Aidha amesema Jeshi la Polisi mkoani Tanga limejipanga vizuri kwa kufanya doria za kutosha, lengo likiwa ni kuhakikisha watu hawafanyi uhalifu.