Polisi kuimarisha ulinzi Kariakoo

0
140

Jeshi la Polisi nchini limewahakikishia wafanyabiashara na wananchi wote wanaofanya shughuli zao za biashara na kupata mahitaji katika eneo la Soko la Kariakoo lililopo mkoani Dar es Salaam kuwa ulinzi utaimarishwa ipasavyo katika maeneo yote ya soko hilo na kwamba linaendelea kuwatafuta watu walioandaa na kusambaza taarifa za kuwepo kwa mgomo kuanzia Jumatatu Juni 24, 2024.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila hofu, na kwa yeyote mwenye changamoto zenye kuhitaji utatuzi afuate utaratibu wa kuzifikisha kwenye mamkaka husika ili zifanyiwe kazi na sio kuvunja sheria kwa kutoa vitisho na kulazimisha wengine kufanya yale ambayo hawakubaliani nayo.

Misime ameyasema hayo kufuatia tangazo linalosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari lenye kichwa cha habari “KUFUNGA BIASHARA ZETU” likiwa na ujumbe unaosema “Wafanyabiashara wote wa viunga vya Kariakoo mnatakiwa kufunga biashara zenu zote ikiwemo maduka yenu, ofisi zetu na chochote unachokifanya kuanzia Jumatatu ya Juni 24, 2024 bila ukomo hadi pale changamoto zetu zote za kibiashara zitakapoweza kutatuliwa”.

Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi nchini amesema mbali na tangazo hilo kutokujulikana limetolewa na nani, limeenda mbali zaidi hadi kukiuka sheria za nchi kwa kutangaza vitisho kuwa; “Wafanyabiashara watakaokaidi agizo hilo mshale wa jicho utakuwa haki yao”.