Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi leo Jumapili, Mei 19, 2024 imemteua Khamis Yussuf Mussa maarufu Pele, kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika Jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo umepangwa kufanyika Juni 8, 2024 na unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ahmada Yahya Shaa aliyefariki dunia Aprili 8, 2024.
Aidha, Kamati Kuu ya CCM, imezipongeza Serikali zake zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Dkt. Husein Mwinyi kwa namna zinavyoendelea kuwatumikia wananchi kwa vitendo kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025.