Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu iliyopo mkoani Dar es salaam, imemwachia huru mfanyabiashara Marijan Msofe maarufu kama Papa Msofe na wenzake wanne baada ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati mahakamani hapo akionesha nia ya kutoendelea na shauri lililokuwa likiwakabili.
Katika kesi ya msingi mshtakiwa Msofe na wenzake wanadaiwa kujipatia zaidi ya shilingi milioni 900 kwa njia ya udanganyifu.
Mbali na Msofe, washtakiwa wengine ni Josephine Haule, Wenceslau Mtui, Mwesigwa Mhina ambaye ni wakili wa kujitegemea na Fadhil Mganga.
Hati hiyo imewasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Huruma Shaidi, ambaye amewaachia huru washtakiwa hao baada ya kujiridhisha na hati kutoka ofisi ya DPP na kusomwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Simon.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kati ya Desemba mwaka 2018 na Septemba mwaka 2019, washtakiwa hao kwa pamoja na wenzao ambao hawajakamatwa walifanya mpango wa kuongoza genge la uhalifu.
Shtaka la pili hadi la mwisho, washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na utakatishaji fedha zaidi ya shilingi milioni 900 Katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2018 na 2019 wakidanganya kumuuzia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Mahson kilogramu 20 za dhahabu ili azisafirishe kwenda nchini Ureno.