Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi imemuhukumu kifungu cha miaka 25 jela mmoja kati ya viongozi wa kikundi cha Waasi cha Lord’s Resistency Army -LRA cha nchini Uganda, – Dominic Ongwen baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na uhalifu wa kivita.
Ongwen alikuwa akituhumiwa kuhusika na mauji dhidi ya raia wa Uganda na katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo LRA imekuwa ikitekeleza mauaji hayo.
Waasi wa LRA, baada ya kuona wanazidiwa nguvu nchini Uganda walikimbilia katika nchi jirani ya Afrika ya Kati, ambako pia wamekuwa wakiendesha vitendo vya ukatili na kisha kukimbilia msituni.
Vitendo vya mauaji na ukatili vilivyokuwa vikitekelezwa na LRA inasemakana vilianza mwaka 1987, kikundi hicho kilipoanza mashambulio dhidi ya Serikali ya Uganda.