Ombi la kufutwa kesi ya kina Sabaya latupwa

0
313

Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imetupilia mbali maombi ya mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne waliotaka kesi hiyo ifutwe kutokana na kuchelewa kwa upelelezi.

Mawakili hao wa utetezi waliwasilisha ombi hilo mahakamani hapo tarehe 12 mwezi huu wakitaka mahakama iwaachie huru watuhumiwa hao na upelelezi uendelee wakiwa huru.

Ombi hilo limetupiliwa mbali na Hakimu Mkazi Mfawidhi Salome Mshasha ambaye amesema kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka wala kibali cha kusikiliza kesi hiyo, haiwezi kutoa uamuzi wowote wala kuamuru upande wa mashtaka kuharakisha kesi hiyo.

Hata hivyo amesema, pamoja na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ni vema upande wa mashtaka ukawa makini kwani mahakama ni chombo cha kutenda haki na wananchi huko nje wanataka kuona hiyo haki ikipatikana.

Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo lla uhujumu uchumi, kuongoza genge la uhalifu pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 12 mwaka huu.