Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo imara na miradi yote ya kimkakati inaendelea kujengwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani nayo.
Akizungumza mkoani Dar es salaam mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo makini na itaendelea kuwatumikia Watanzania.
Amesema kinachotakiwa kwa Watanzania hivi sasa ni kutumia muda wao mwingi kufanya shughuli za maendeleo kuliko mambo mengine yasiyo na tija.
Kuhusu mradi huo wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Magomeni Kota, Waziri Mkuu Majaliwa amesema amefurahi kukuta majengo yamekamilika na kwamba ameridhika na maendeleo ya ujenzi wake.
Ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha unakamilisha kazi iliyosalia haraka iwezekanavyo ili mwaka huu wananchi waanze kuishi kwenye nyumba hizo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, -Daud Kondoro amesema mradi huo una jumla ya majengo matano yenye uwezo wa kukaliwa na familia 656.
Amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo za makazi, pia katika eneo hilo wanajenga maduka makubwa pamoja na vizimba kwa ajili ya wajasiriamali.
Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2016 kwa gharama ya shilingi bilioni 50, na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 94.
Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo za makazi za Magomeni Kota, Waziri Mkuu Majaliwa amekagua kituo cha reli ya kisasa cha Tanzanite kilichopo mkoani Dar es salaam.