NGOs zinazokiuka sheria zaonywa

0
233

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali haitavumilia kuona mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi bila kufuata sheria.

Dkt. Gwajima amesema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji na uratibu wa mashirika hayo yasiyo ya Kiserikali ili yatoe mchango chanya katika ujenzi wa Taifa na kwamba shilingi milioni 585.5 zimetengwa  kwa ajili ya ufuatiliaji wa mashirika yasiyo ya Kiserikali elfu moja Tanzania Bara.

Waziri huyo wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kuwa, pamoja na jitihada zinazoendelea kufuatilia na kuratibu shughuli za mashirika hayo, Serikali itahakikisha jitihada zaidi zinaongezeka ili kuyabaini mashirika yasiyotimiza masharti.

” Sitokubali kuona Shirika lolote lisilo la kiserikali linafanya kazi bila kusajiliwa kwa mujibu wa sheria, sitovumilia hili litokee jisajilini mfanye kazi kwa utaratibu” amesema Waziri Gwajima.

Akizungumzia umuhimu wa makundi maalum katika jamii wakiwemo Watoto, Wazee na Wenye ulemavu, Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za ustawi wa jamii, kuboresha huduma kwa Wazee, kufuatilia na kuimarisha uanzishaji wa vituo vya kulea watoto wadogo na kuboresha huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia.

“Niseme jumla ya shilingi bilioni 12.4 zimetengwa kwa ajili hiyo ikiwemo kukarabati majengo na miundombinu katika makazi 10 ya wazee ili kuwezesha kuwa na mazingira mazuri ya kulea wazee na wasiojiweza,” amesema Waziri Gwajima.