Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mwita Waitara ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwekeza katika utoaji wa elimu na kuacha kutoza faini mara kwa mara kwa wananchi.
“Changamoto mliyonayo kubwa ni kwamba mnatoza faini sana. Wekezeni katika kutoa elimu kwa watu, ili waelewe vizuri masuala ya mazingira. Sehemu kubwa ifanyeni katika elimu na ushirikishwaji, suala la mazingira lizungumzwe kwa ukubwa wake,” amesema Waitara akiwa ziarani Dar es Salaam.
Aidha, amelitaka baraza hilo kuwatoza faini wale wote wanaofungua mabomba ya vyoo na kutiririsha maji yasiyo salama kwenye makazi ya watu pindi waonapo mvua inanyesha kwa maelezo kuwa ni kitendo cha kinyama.
Hata hivyo Waitara amefurahishwa na ujenzi wa kiwanda cha kusindika taka unaofanywa na Manispaa ya Kinondoni, ambapo amesema kitasaidia manispaa hiyo kuwa salama na safi.
“Nimeambiwa kiwanda hiki kitatoa mbolea ya mboji kwa taka ambazo zinatokana na matunda na mbogamboga, huu mradi utasaidia manispaa kuwa salama na safi lakini pia ni sehemu ya kipato kwa sababu mbolea itakayopatikana hapa itasaidia kuongeza kipato katika manispaa. Kwa hiyo tunatarajia kwamba manispaa nyingine zitaiga mfano huu,” amesema Waitara.
Awali akizungumza kuhusu utendaji kazi wa baraza hilo, Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Dkt. Menani Jandu amesema changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na idadi ndogo ya wafanyakazi na hivyo kuwa changamoto kukabiliana na idadi ya miradi inayosajiliwa ambayo ni kati ya 1,500 na 1,700 kwa mwaka.
Akitoa taarifa ya mazingira, Mkuu wa Idara ya Mazingira katika Manispaa ya Ubungo, Lawi Benard amesema kuwa wanazalisha taka ngumu tani 828 kwa siku huku wakiwa na magari matatu tu ya kuzolea taka jambo ambalo linawawia vigumu kuzoa taka zote.
Takribani tani 1,223 huzalishwa kwa siku katika Manispaa ya Kinondoni sawa na tani 446,614 kwa mwaka ambapo uwezo wa halmashauri na wadau wengine kuzoa ni sawa tani 263,502 kwa mwaka sawa na asilimia 59.