NEC yatangaza uchaguzi katika kata nne

0
1201

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo  katika kata mbili utakaofanyika Januari 19  mwaka 2019, uchaguzi utakaofanyika pamoja na ule wa jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam  na kata 46 za Tanzania Bara uliotangazwa hapo awali.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk amezitaja kata hizo kuwa ni Mwanahina iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga  na Kata ya Biturana katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Amesema kuwa fomu za uteuzi wa wagombea hao zitatolewa kati ya Disemba 21 na 27 mwaka huu na uteuzi wa wagombea utafanyika Disemba 27 mwaka huu,  huku kampeni za uchaguzi huo mdogo wa udiwani zikipangwa kuanza  Disemba 28 mwaka huu hadi Januari 18 mwaka 2019.

Jaji Mbarouk ametoa wito kwa  vyama vya siasa nchini  kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo wa udiwani.