NEC yatakiwa kuharakisha uboreshaji daftari la wapiga kura

0
319

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeendelea na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya kwanza.

Akiahirisha Bunge jijini Dodoma leo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, hadi Februari pili mwaka huu, NEC ilikua imekamilisha uandikishaji wa wapiga kura katika kanda ndogo 12 kati ya 14 zilizopangwa katika ratiba ya uboreshaji wa awamu ya kwanza.

Amezitaja kanda hizo ndogo zilizokamilisha zoezi hilo kuwa ni  pamoja na zile zinazohusisha mikoa 22 ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga.

Mingine ni Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Singida, Dodoma, Songwe, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Njombe, Lindi, Mtwara, Tanga na Morogoro katika wilaya za Ulanga na Malinyi pamoja na Zanzibar.

“Uandikishaji wa wapiga kura ni wa siku saba kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, aidha zoezi la uboreshaji linahusisha uandikishaji wa wapiga kura wapya ambao hawajahi kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura, urekebishaji wa taarifa za wapiga kura walioandikishwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa ikiwemo kufariki,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka NEC iharakishe zoezi la uandikishaji na amewataka wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kwa wingi ili kuboresha taarifa zao na kujiandikisha upya kwa wale wenye umri wa miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Bunge limeahirishwa hadi Machi 31 mwaka huu.