Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Ndejembi amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama kumchukulia hatua za kinidhamu Mhandisi Ujenzi wa Halmashauri hiyo, Daniel Kileo kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa ya mradi wa BOOST.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa madarasa akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi inayojengwa na Serikali kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP.
“Mkurugenzi mchukulie hatua za kinidhamu Mhandisi wa Ujenzi na mkaimishe mwingine kwani huyu ameshindwa kusimamia ujenzi wa madarasa na Ofisi ya Rais TAMISEMI itakuletea mhandisi mwingine atakayesimamia miradi ya ujenzi ya miundombinu ya elimu,” amesema Ndejembi.
Amesema amepewa taarifa kuwa katika Shule ya Sekondari Ashira bweni moja halijajengwa licha ya kuwa fedha zilitolewa na Serikali na Mhandishi huyo kushindwa kusimamia ujenzi huo.