Ndege za Rais kuanza kusafirisha abiria hivi karibuni

0
276

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Ndege Tanzania –Atcl, Ladislaus Matindi amesema wataanza kuzitumia ndege mbili aina ya Foca waliozopewa na rais Dkt. John Magufuli kwa matumizi ya kubebea abiria kutokana na ndege hizo kuwa na mfumo unaoruhusu kubadilishwa matumizi yake.

Matindi amesema hayo katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Tbc one, wakati akielezea mikakati ya shirika hilo kufuatia ujio wa ndege ya pili aina ya Air bus 220-300 na kubainisha kuwa ndege mbili walizopewa na rais aina ya Foca, zitafanyiwa marekebisho ya mfumo na watalaam wa ndege hapa nchini ili zianze kutoa huduma mapema.

Kuhusu matengenezo ya ndege mbli za bombadier q400, Matindi amesema ndege hizo zinafanyiwa marekebisho ikiwa ni utaratibu wa kawaida baada ya kufikisha idadi ya kilometa ili kuboresha ufanisi wake.

Aidha Matindi amebainisha kuwa shirika hilo limefanya utafiti wa kina ili safari zote zinazofanywa na ndege zake zilete tija na faida kwa shirika hilo katika safari za ndani na nje ya nchi.