Nchimbi awatembelea waathirika maporomoko Mbeya

0
174

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na msafara wake, leo Aprili 17, 2024, amewajulia hali na kuwapatia pole wananchi wa Kata ya Itezi, Wilaya ya Mbeya Mjini, walioathiriwa na maporomoko ya udongo na tope kutoka Mlima Kawetele.

Mbali ya kuwasilisha salamu za pole za Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa waathirika hao, Dkt. Nchimbi, kwa niaba ya CCM, amewapatia fedha taslimu ya shilingi milioni 10.

Wananchi hao ambao kwa sasa wamepewa makazi ya muda katika Shule ya Msingi Tambuka Reli, Mbeya Mjini, wameshukuru kwa hatua za chama na serikali kuendelea kuwa nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu.

Dkt. Nchimbi amewataka kuwa na subira wakati huu ambao Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina juu ya tukio hilo ili kujua hatua stahiki za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuzuia maafa hayo yasitokee tena.