Nchi za SADC zatakiwa kuongeza mapambano dhidi ya corona

0
196

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza mapambano dhidi ya virusi vya corona ambavyo vimeenea katika nchi mbalimbali.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC, mkutano unaofanyika kwa njia ya video.

Amesema kwa nchi za SADC ambazo tayari zina wagonjwa wa corona ni muhimu zikahakikisha ugonjwa huo hauenei, na kwa zile ambazo bado hazina maambukizi zihakikishe virusi hivyo haviingii katika nchi hizo.

Pia amezitaka nchi za SADC kushirikiana ili malengo ya kuwepo kwa jumuiya hiyo yaweze kufikiwa.

Ajenda sita zinajadiliwa katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC ambao unafanyika kwa muda wa siku mbili.

Ajenda hizo ni pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya SADC, mpango mkakati wa maendeleo wa SADC katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2030, na hali ya michango na fedha kwa jumuiya hiyo.