NCCR-Mageuzi yatangaza jina la mgombea wa Urais 2020

0
801

Chama cha NCCR-Mageuzi kimemtangaza Abubakar Juma Abubakar kuwa mgombea Urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2020.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Evarist Komu amemtaka mgombea huyo kupeperusha bendera ya chama kwa kusimamia misingi ya chama hicho ambayo ni pamoja na kutetea utu, haki, udugu, usawa na upendo kwa mustakabali wa chama na Watanzania kwa ujumla.

Abubakar ameahidi kusimamia misingi ya chama chake na kuweka mazingira yatakayokuwa chachu ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

Komu amesema hadi sasa wanachama 232 wamechukua fomu za kuomba kugombea ubunge na zaidi ya 3,000 wamechukua fomu za kuomba kugombea udiwani.

Awali, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye amesema chama hicho kitaendesha siasa za kistaarabu wakati wa kampeni za Urais ambapo wagombea wa chama hicho watatakiwa kunadi sera za chama ikiwemo namna ya kudumisha misingi ya chama pamoja na kusimamia amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo na ustawi wa jamii ya Watanzania.