Naibu Spika wa Bunge la Malawi aanza ziara nchini

0
256

Naibu Spika wa kwanza wa bunge la Malawi Madalitso Kazombo yupo nchini kwa ziara ya kikazi.ya siku tano pamoja na mafunzo ya namna ya uendeshaji wa shughuli za bunge.

Akizungumza jijini Dodoma baada ya kupokelewa na mwenyeji wake Naibu Spika wpa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Kazombo licha ya kutoa pole kwa kifo cha Rais wa Serikali ya awamu ya Tano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amesisitiza umuhimu wa bunge kuendelea kuwa kitovu cha demokrasia na uchumi.

Naibu Spika Kazombo amesema bunge la Tanzania na Malawi wamekuwa na mahusianao ya muda mrefu, na ujio wake pamoja na ujumbe wake utawezesha kubadilishana uzoefu.

Akiwa hapa nchini, kiongozi huyo atakutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na kuhudhuria kikao cha bunge na pia atatembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ule wa kimkakati wa ujenzi wa reli ya kisasa.

“Tumekuja hapa kujifunza jinsi Tanzania walivyoweza kufanya uchumi kuwa endelevu,” ameeleza Naibu Spika huyo wa Kwanza wa Bunge la Malawi.

“Tanzania ni kitovu cha amani sehemu ya kusini mwa Afrika, namna gani bunge limeweza kuchangia katika viwanda na wakati huohuo kueleza namna gani Malawi imefanya, kumbuka tulikuwa na uchaguzi mzuri uliopita na bunge la Malawi lilichukua hatua muhimu kuhakikisha kipindi cha mpito kinapita kwa amani bila vita, kwa hiyo kumekuja hapa kuhakikisha sote kati yetu ni kwa namna gani tunahakikisha watu wetu wanafurahia demokrasi, “ameongeza Kazombo.