Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesikitishwa na utendaji mbovu wa kazi wa watumishi wa Wakala wa Maji Vijijini(RUWASA) Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutoa taarifa za uongo na kutelekeza miradi licha ya serikali kutoa fedha.
Akitoa taarifa mbele ya Naibu Waziri katika ziara yake ya kutembelea Wilaya ya Mbarali Meneja wa Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) Wilaya hiyo Job Mwakasala amesema upatikanaji wa maji ni asilimia 66.96 na Rujewa asilimia 67.4 na pia kuna miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwemo tisa ya vijijini na mmoja wa mjini.
Mwakasala amesema mradi wa Ruduga Mawindi unatekelezwa kwa awamu tangu 2014/2015 ambao utavifikia vijiji sita utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi na mbili ambapo mpaka sasa umetumia zaidi ya shilingi bilioni nne.
Taarifa hiyo ya upatikanaji wa maji ilipingwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune ambaye alisema maji yanayopatikana kwa mgao ni chini ya asilimia thelathini pia watendaji wa RUWASA hawana ushirikiano.
Mfune amesema mradi huo umechukua zaidi ya miaka saba na bado unasua sua licha ya fedha kutolewa na serikali.
Akitoa hotuba yake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesikitishwa na utendaji mbovu wa Mhandisi Job Mwakasala kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi ya miradi na kutelekeza mabomba ya mradi wa Ruduga Mawindi tangu mwezi August mwaka jana na kuagiza aondolewe kwenye Mradi huo na apangiwe kazi nyingine.