Naibu Waziri wa Afya atumbua wawili, wengine wakiwekwa rumande

0
396
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia moja ya jalada la mgonjwa katika wodi ya wanawake katika Hospitali ya Tukuyu wakati wa ziara yake wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ngugulile ameagiza kuwekwa ndani na kutolewa katika nafasi zao Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Tukuyu, Manase Ngogo na Afisa Ugavi, Vumilia Mwaijande kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wao.

Pia, Dkt. Ndugulile ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani mfamasia na afisa manunuzi wa hospitali hiyo kutokana na usimamizi mbovu wa stoo ya dawa na kukosekana kwa taarifa sahihi za dawa zinazotoka na zinazoingia katika stoo hiyo.

Ametoa agizo hilo wilayani Rungwe mkoani Mbeya wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya Tukuyu na kujionea utendaji mbovu wa hospitali hiyo katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Nilishapata taarifa za wizi wa dawa Tukuyu sasa hili linathibitisha hilo, huwezi ukamuweka afisa ugavi asimamie stoo ya dawa wakati mfamasia yupo” alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Nduguile amewapa onyo mganga mkuu wa Wilaya ya Rungwe, muuguzu mkuu wa wilaya na mfamasia wa hospitali na kuwatahadharisha na utendaji wao wa kazi kwani umekuwa sio wa kuridhisha na ameahidi kuwaangalia kwa karibu zaidi.

“Katika ziara zangu zote sijawahi kuona utumbo kama huu, niseme tu sijaridhishwa na utendaji wenu kabisa na mganga mkuu wa mkoa chukua hatua Wilaya ya Rungwe hatufanyi vizuri katika sekta ya afya tunamuangusha Rais Magufuli,” alisema Dkt. Ndugulile

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Rungwe Mnkondo Bendera amesema kuwa kama wilaya hawawezi kuvumilia uozo wa watoa huduma za afya kwani wataendelea kuangalia kwa karibu sekta ya afya na watakaogundulika wanahujumu sekta hiyo watachukuliwa hatua kali.

“Kwakweli hatutavumilia haya kama ninyi wasaidizi wetu katika sekta ya Afya mna mbinu za kutuhujumu katika jitihada za serikali kutoa huduma bora za afya kwa wananchi basi tutawashughulikia ipasavyo,” alihitimisha Bendera.