Mwili wa Mbunge Martha Umbulla wapokelewa Dodoma

0
239

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo ameshiriki katika mapokezi ya mwili wa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Martha Umbulla katika uwanja wa ndege jijini Dodoma.
 
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Martha Umbulla alikuwa na mchango mkubwa Bungeni, hasa katika kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali. 
 
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amewaomba ndugu, jamaa, marafiki na Wabunge kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na wamuombee ili Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi.
 
Akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa jimbo la Urambo mkoani Tabora Magreth Sitta, amewataka Wabunge wenzake kuishi na kuenzi yale yote mazuri ambayo Martha alikuwa akifanya kwani alikuwa mbunge makini.
 
Awali Waziri Mkuu Majaliwa alisaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
 
Mbunge Martha Umbulla alifariki dunia tarehe 21 mwezi huu katika hospitali ya HCG Mumbai nchini India, alipokuwa akipatiwa matibabu.