Mwili wa JPM wapokelewa Dodoma

0
184

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli umewasili mkoani Dodoma jioni ya leo ukitokea mkoani Dar es salaam, ambapo kwa siku mbili mfululizo mwili huo umeagwa na Wakazi wa mkoa huo.

Ndege iliyobeba mwili wa Dkt Magufuli,-Airbus 220-300 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imewasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma majira ya saa 12 jioni na kupokelewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali.

Mara baada ya kuwasili mkoani Dodoma mwili wa Dkt Magufuli umepelekwa katika Ikulu ya Chamwino na umepita katika barabara za Chako ni chako, Nyerere, Jamatini, Morena na Buigiri.

Kesho asubuhi, mwili wa Dkt Magufuli utaagwa kwa heshima za kibunge katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha itafuata shughuli ya kuuaga Kitaifa itakayofanyika katika uwanja wa Jamhuri.