Mwili wa mchimbaji mdogo wa madini Bahati Ngalaba aliyefukiwa na kifusi cha udongo kwa muda wa siku saba katika mgodi wa Golden Hainga, Kata ya Nyarugusu Wilaya ya Geita umepatikana.
Bahati aliyefukiwa na kifusi Aprili 26, 2024 akiwa na mwenzake ambaye alifanikiwa kutoka akiwa hai, mwili wake umepatikana kufuatia jitihada zilizofanywa na
askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokojaji mkoani Geita kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.
Bahati Ngalaba na mwenzake Nestory Anthony waliingia katika duara lililopo kwenye mgodi huo na ndipo kifusi kikashuka kutoka duara jingine na kuwafukia.
Akizungumza na TBC Digital Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Hamisi Dawa ametoa rai kwa wenye miduara mkoani humo kuacha shughuli za uchimbaji madini katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.