MWENGE WAKATAA KUZINDUA MRADI WA MAJI CHIPOLE

0
109

Mwenge wa Uhuru umekataa kuzindua mradi wa maji wa Chipole uliopo katika kijiji cha Chipole halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Luteni Josephine Mwambashi amesema mradi huo ambao umegharimu shilingi milioni 365 umebainika kuwa na kasoro nyingi .

Amesema taarifa ya mradi huo iliyotolewa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) halmashauri ya mji wa Masasi inaoneesha mradi umetumia shilingi milioni 400, jambo ambalo siyo kweli.

Kasoro nyingine ya mradi huo ni udanganyifu uliofanyika kwenye ununuzi wa mabomba ambapo taarifa inasema yamenunuliwa 20 huku yaliyonunuliwa yakiwa 19.

Amesema katika mradi huo kuna upotevu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 30, ambazo hazijulikani zilipo.

Kufuatia kasoro hizo zilizobainika kwenye mradi huo wa maji wa Chipole , Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Luteni Mwambashi amezikabidhi nyaraka zote za mradi huo kwa mkuu wa wilaya ya Masasi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) ili uchunguzi wa mradi huo uanze mara moja.

Mradi huo wa maji wa Chipole ulianza kutekelezwa mwezi Mei mwaka 2020 na kukamilika mwezi Februari mwaka huu, na tayari umeanza kufanya kazi .