Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Luteni Josephine Mwambashi amekataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea kilichopo Mabwepande wilayani Kinondoni mkoani Dar es salaam.
Luteni Mwambashi amesema Mwenge wa Uhuru hauwezi kuzindua mradi huo kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka zonazoonesha matumizi ya shilingi milioni 800 zilizolipwa na Manispaa ya Kinondoni katika mradi huo.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa amesema wamepata nyaraka moja yenye thamani ya shilingi milioni 10 kati ya shilingi milioni 800 zilizotolewa na Manispaa ya Kinondoni kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.
Ameongeza kuwa licha ya ufadhili kutoka Hamburg nchini Ujerumani lakini fedha za ndani pia zimetumika lakini hazioneshi vielelezo vya namna zilivyotumika.
Amemtaka Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Kinondoni kuchunguza matumizi hayo na kumpa taarifa kabla mwenge huo haujatoka mkoa wa Dar es Salaam.