Mwanamke Mtanzania atwaa Tuzo ya LUCE 2024

0
284

Mhandisi Joyce Kisamo kutoka Wizara ya Nishati amekuwa Mwafrika wa pili kutwaa Tuzo ya LUCE ya Mwanamke aliyefanya vizuri katika nishati, mazingira na sekta endelevu.

Mhandisi Joyce Kisamo ambaye ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Petroli kutoka Wizara ya Nishati ameibuka mshindi katika Tuzo za LUCE 2024 kwenye kundi la Mwanamke mwenye uzoefu na aliyeacha alama, na kuwashinda Wanawake wengine 15 kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya na Asia.

Zaidi ya kura 2,000 zilipigwa duniani kote na kura 600 zilimpa ushindi Mhandisi Joyce ambaye alikuwa mwafrika pekee na katika kinyang’anyiro hicho ameibuka mshindi kwa kuacha alama nyingi katika utendaji wake wa kazi.

Kwa ushindi huo Mhandisi Joyce ametambulika Kimataifa kuwa Mwanamke mwenye uzoefu, aliyefanyakazi na kuacha alama zenye manufaa kiuchumi, kimazingira na kijamii katika sekta endelevu hususani nishati safi na endelevu.

Makabidhiano ya tuzo hiyo iliyotolewa na
mpango wa Lights on Women kwa ushirikiano na Landwärme na Edison, yamefanyika huko Florence nchini Italia.