Mwanafunzi amuandikia barua Mwalimu wake ya kukataa shule

0
342

Mwanafunzi mmoja aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Msimbati iliyopo wilaya ya Mtwara amemuandikia barua mkuu wa shule hiyo ya kukataa kusoma shule.

Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Hamisi Sadala akizungumza kwenye kikao kazi kilichowakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari halmashauri wilaya ya Mtwara, amethibitisha kupokea barua hiyo na kusema alikabidhiwa February 22 saa mbili usiku kutoka kwa mwanafunzi huyo.

Sadala amesema mtoto huyo ameiandika barua hiyo akiwa na wazazi wake baba na mama ambao wote wanafahamu kuwa mtoto wao ameandika barua ya kukataa shule lakini hawakuchukua hatua yoyote na badala yake wameridhika na hatua iliyochukuliwa na mtoto wao.

Amefafanua kuwa kuna vijana walitakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka jana na mwaka huu kuingia kidato cha pili hawakuripoti shule kwa kipindi hicho ambao kwa sasa wanajishughulisha na masuala ya uvuvi pwani jambo ambalo limemvutia kijana huyo na kwenda kujiunga na vijana hao.

Mwalimu Sadala amesema kaka wa kijana huyo anasoma kidato cha pili katika shule hiyo na alipoulizwa na mkuu huyo wa shule kwa nini mdogo wako hataki kusoma akasema mdogo wake anapenda kuvua samaki pwani kwa kuwa kuna vijana wenzake wanajishughulisha na uvuvi.