MV Malagarasi yasombwa na maji, abiria watoka salama

0
878
Muonekano wa kivuko cha MV. Malagarasi kilichopo katika eneo la Ilagala mkoani Kigoma. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100, magari sita na tani 50 kwa wakati mmoja.

Kivuko cha MV Malagarasi kilichopo katika Mto Malagarasi, Kata ya Ilagala, wilayani Uvinza mkoani Kigoma kimepata hitilafu na kusombwa na maji.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa kivuko hicho kimesombwa na maji hadi Kijiji cha Karago kikiwa na abiria 33 na kwamba wote wametoka salama.

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko akitoa maelekezo baada ya kufika eneo la tukio.

Kufuatia tukio hilo Mrindoko amepiga marufuku wananchi kuvuka mto huo kwa kutumia chombo chochote cha usafiri mpaka hapo serikali itakaporejesha huduma nyingine.

Kukosekana kwa huduma ya kivuko katika eneo la Ilagala wilayani Uvinza kumekatisha mawasiliano ya kwenda katika Kata za Sunuka, Sigunga, Herembe, Igalula, Buhingu, Kalya, na Kijiji cha Kajeje.