Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iko mbioni kupeleka Bungeni Muswada utakaowezesha kutungwa kwa sheria ya kulinda taarifa binafsi, lengo likiwa ni kulinda faragha na taarifa za Mwananchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge kwenye semina kuhusu huduma za mawasiliano na intaneti.
Amesea sheria hiyo inaandaliwa ili kulinda faragha na taarifa binafsi za Wananchi katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa, usafirishaji, matumizi na utunzaji wa taarifa hizo.
Dkt. Ndugulile amewataka Wabunge kuwa tayari pindi pendekezo la muswada litakapowasilishwa Bungeni, ili sheria hiyo iweze kutungwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Hivi sasa ujambazi umehama kutoka silaha za mkononi na kuhamia mtandaoni, Serikali itaendelea kuelimisha Wananchi, kuboresha mifumo na teknolojia ili nchi iwe mbele zaidi katika kudhibiti uhalifu mtandaoni,” amesisitiza Dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso ameishauri Serikali iongezee fedha za kuuwezesha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa ruzuku ya kutosha kwa kampuni za simu ili mawasiliano yafike kwa Wananchi wote, ikiwa ni pamoja na kuongeza usikivu wa redio kwenye maeneo ya mpakani.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Akson ameipongeza wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuwapatia.semina hiyo.