Muswada wa Huduma ya Habari kesho bungeni

0
208

Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 utasomwa kwa mara ya kwanza hapo kesho bungeni jijini Dodoma.

Hatua ya kusomwa kwa muswada huo imetangazwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye jijini Dodoma.

Waziri Nape amewaambia waandishi wa habari kuwa kusomwa kwa muswada  huo ambao hapo jana serikali kupitia kwa Msemaji wake Mkuu Gerson Msigwa ilitangaza kuahirishwa kusomwa kwake, kumetokana na mabadiliko ya kusomwa kwa muswada wa Bima ya Afya kwa Wote.

Hapo jana baada ya serikali kutangaza kushindwa kusomwa kwa muswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari kutokana na ratiba ngumu ya vikao vya bunge, Jukwaa la Wahariri Tanzania lilitoa taarifa yake iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa jukwaa hilo Deodatus Balile likilalamikia kile ilichosema ni kupigwa danadana kusomwa kwa muswada huo toka mwezi Februari mwaka 2022.

Akijibu malalamiko hayo, Waziri Nape amesema serikali  ina nia ya dhati ya kutekeleza marekebisho hayo na amewataka wadau wote wa mchakato huo kuiamini.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, pamoja na muswada huo kuingia bungeni kwa mara ya kwanza hapo kesho, mchakato wake huenda ukachukuwa muda mrefu kutokana na michakato mbalimbali ndani ya bunge ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya kamati za bunge.