Mufti wa Tanzania Dkt. Abubakar Zubeir amewataka watu wote waliopoteza wapendwa wao katika ajali iliyotokea wilayani Korogwe mkoani Tanga pamoja na Watanzania wote kuwa na moyo wa uvumilivu huku wakimtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila jambo wanalolifanya iwe kwenye huzuni au furaha.
Mufti ametoa kauli hiyo katika viwanja vya hospitali ya wilaya ya Korogwe, Magunga wakati wa ibada ya kuaga miili ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo.
Watu 20 wamefariki dunia katika ajali hiyo, ambapo wengi wao ni wa familia moja waliokuwa wakisafiri kutoka mkoani Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro kwenye mazishi ya ndugu yao.