Mtoto wa siku saba aibwa hospitalini

0
418

Mwanamke mmoja amepoteza mtoto wake mwenye siku saba baada ya kumpa mtu amshike alipokuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iringa, Frelimo, alikokwenda kwa ajili ya huduma ya afya.

Daktari mkuu wa hospitali hiyo, Pili Zambi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi majira ya saa 7 mchana baada ya mama mzazi huyo kumpa mwanamke mmoja amshike mwanae wakati yeye akipeleka mizigo kwenye wodi ya wazazi, baada ya kutakiwa kufanya hivyo.

Dkt. Zambi amesema kuwa mama huyo aliporudi hakumkuta mwanamke aliyempa mtoto wala mwanae na jitihada za kumtafuta hazikuzaa matunda.

Baada ya jitihada za kumpata kukwama, Dkt. Zambi aliripoti tukio hilo polisi kwa uchunguzi zaidi.

Kutokana na tukio hilo ambalo ni la kwanza kutokea katika hospitali hiyo, Dkt. Zambi amewataka watu wanaofika hapo kupata huduma kutokumuamini kila mtu.