Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetoa fursa kwa wahitimu 2,194 wa elimu ya msingi waliofutiwa matokeo kutokana na udanganyifu, kufanya mtihani wa marudio.
Mtihani huo wa marudio umepangwa kufanyika tarehe 21 na 22 mwezi huu.
NECTA imesema watahiniwa ambao shule zao zimefungiwa kuwa vituo vya mitihani, watafanya kwenye vituo vya jirani na shule zao.
Mtihani huo wa Marudio utaendeshwa kwa kusimamiwa na kamati za uendeshaji mtihani za mikoa husika kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uendeshaji mitihani ya kitaifa.
Desemba Mosi mwaka huu NECTA ilitangaza matokeo ya darasa la saba, ambapo shule 24 zilifungiwa kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi iliyofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu.