MTANZANIA WA PILI AUAWA ISRAEL

0
576

Mtanzania wa pili abainika kuuawa na kundi la Hamas

Serikali ya Israel imeijulisha Tanzania kuwa Mtanzania Joshua Mollel aliyekuwa anasoma nchini Israel aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas 7 Oktoba 2023.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ambapo ameeleza kuwa “kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa awali wa kuwapeleka Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja na Afisa wa Serikali nchini Israel, kuungana na Balozi wetu na maafisa waliopo huko, kukutana na kuzungumza na mamlaka za nchi hiyo ili kupata taarifa za ziada.”

Joshua alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania 260 waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

Yeye na mwenzake Clemence Mtenga walitekwa na kuuawa na kundi hilo mara baada ya kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israel, ambayo Mtenga alizikwa Novemba 28 mwaka huu katika Kijiji cha Kirwa, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.