Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefanikiwa kuboresha huduma za afya kwa magonjwa yasiyoambukiza, ambapo takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa magonjwa hayo ndio yaliyoongoza kwa kusababisha vifo kwa asilimia 33 nchini huku vifo vya magonjwa ya moyo vikiwa ni asilimia 13.
Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo mkoani Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mtambo mpya wa uchunguzi na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo Tanzania ni nchi ya nane Barani Afrika kwa kuwa na mtambo wa aina hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan pia ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi inayoifanya katika kuokoa maisha ya Watanzania na kuahidi kufanyia kazi changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na maslahi ya Watumishi.
Pia ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika endapo Wagonjwa wa moyo nchini wangeenda kutibiwa nje ya nchi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Profesa Mohamed Janabi alieleza kuwa mwaka 2020 Serikali ilitoa shilingi bilioni 4.6 kwa taasisi hiyo ili inunue mtambo huo, na kwamba kabla ya mwaka 2025 fedha hiyo itakuwa imerudi kutokana na mapato yatakayopatina kutokana na mtambo huo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroty Gwajima amesema mkakati wa wizara yake ni kuifanya Tanzania kuwa kitivo cha utalii wa tiba.