Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Muhonda, Zawadi Sanga ametoa wito kwa walimu wa shule za sekondari waliopatiwa mafunzo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutumia elimu hiyo kutatua changamoto zilizopo ngazi ya awali.
Akitoa mafunzo katika Chuo cha Ualimu Monduli mkoani Arusha wakati wa semina iliyokutanisha walimu wa shule za sekondari kutoka mikoa ya Tanga na Manyara, Sanga amesisitiza elimu waliyoipata walimu hao ikawavushe wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na isisababishe kuingilia kazi za maafisa TEHAMA.
Amesema katika halmashauri wapo maafisa TEHAMA ambao wana jukumu la kushughulika na changamoto zinazohitaji utaalamu zaidi katika utatuzi wake na ikiwa watakutana na changamoto zinazohitaji utaalamu zaidi basi wafuate hatua za mawasiliano ya kuripoti changamoto hiyo katika ngazi husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi ili wasivuke mipaka.
Sanga amewakumbusha walimu hao mambo kadhaa wanayoweza kuyafanya wakati wa kutatua changamoto wanazokutana nazo kama hatua za awali ambayo ni pamoja na kuunganisha kompyuta kwa ajili ya matumizi yao na kutekeleza taratibu za msingi katika vifaa vya TEHAMA kama vile kuweka programu tumizi walizopatiwa na Ofisi ya TEHAMA katika vifaa wanavyotumia.
Semina hiyo ambayo inatekelezwa chini ya Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), inaendelea katika Chuo cha Ualimu Monduli ambapo kundi la kwanza la waliopatiwa mafunzo hayo ni walimu 431 kutoka mikoa ya Tanga na Manyara.