Msitishwe na corona, chapeni kazi: Rais Magufuli

0
508

Rais John Magufuli amewataka Watanzania kutotishwa na virusi vya corona na badala yake waendelee kuchapa kazi na kujenga uchumi.

Rais Magufuli amesema hayo alipojumuika na Waumini wengine wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu la Dodoma katika Ibada iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Onesmo Wissi.

Hata hivyo Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuzingatia tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya ili kujikinga kuambukizwa virusi hivyo vya corona.

Amesema kuwepo kwa homa ya corona nchini isiwe sababu ya kutishana kiasi cha kumsahau Mwenyezi Mungu, hivyo ametoa wito kwa Waumini wa dini ya Kikristo na wale wa madhehebu mengine nchini kumrudia Mwenyezi Mungu ili aliepushe Taifa na virusi hivyo.

Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya homa ya corona ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na badala yake ametaka Watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakizingatia tahadhari.

“Watu tusitishane, tunatishana mno, niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu” amesema Rais Magufuli.

Amewashukuru viongozi wa dini zote nchini kwa kuungana na serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aliepushe na homa ya corona.