Msimu wa soko la Tumbaku wazinduliwa Malawi

0
259

Rais John Magufuli amewashauri wakulima wa zao la Tumbaku nchini Malawi,  kutochafua tumbaku yao kwa kuweka vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mawe kwa lengo la kuongeza uzito wakati wa mauzo.

Rais Magufuli ametoa ushauri huo mjini Lilongwe nchini Malawi,  wakati wa ufunguzi wa msimu wa Soko la Tumbaku, na kuwataka Wakulima hao wasisite kuuza tumbaku yao kwa bei ya juu licha ya kuwepo kwa utaratibu wa Tumbaku hiyo kuuzwa kwa bei elekezi.

Akizungumza na Wananchi mbalimbali wa Malawi waliohudhuria uzinduzi huo, Rais Magufuli ameongeza kuwa  upo umuhimu kwa nchi ya Malawi na hata Tanzania kuongeza viwanda vya usindikaji wa Tumbaku, kwani kwa kufanya hivyo Tumbaku itakua na faida zaidi kwa mkulima.

Awali akizungumnza wakati wa uzinduzi huo wa msimu wa Soko la Tumbaku nchini Malawi, Rais Arthur Peter Mutharika wa nchi hiyo amesema kuwa lengo la serikali ya nchi hiyo ni kuhakikisha kuwa mkulima wa Tumbaku anafaidika na zao hilo.

Amesema kuwa kwa kuzingatia jambo hilo, ndio maana umeandaliwa utaratibu maalumu wa uuzaji wa zao hilo na kwamba serikali ya Malawi itahakikisha hakuna mkulima atakayenyonywa wakati wa kuuza tumbaku yake.