MSD kuja na mkakati wa kuboresha huduma za afya

0
167

Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati Dodoma imekutana na wadau na wateja wake wakiwemo waganga wakuu, wafamasia na watendaji wa Halamshauri kuhakikisha wanajadili uboreshaji wa huduma za afya na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa uhakika kupunguza kero kwa wananchi.

Akizungumza na wadau hao wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi amesema lengo la bohari kurejesha mikutano hiyo ya pamoja na wadau ni kukubali kukoselewa, kujenga mazingira ya kupunguza changamoto za pande zote mbili, kubadilishana uzoefu na kukubaliana kufanya kazi kwa pamoja bila kutafuta mshindi kwa kuwa wote wanamuhudumia mwananchi wa Tanzania.

Amesema lengo kikao kazi hicho ni kuhakikisha wanajadili uboreshaji wa huduma za afya na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa uhakika kupunguza kero kwa jamii.

Kwa upande wake Katibu Tawala  wa Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu,  amesema katika kikao hicho kilichoshirikisha watendaji wenye ngazi ya maamuzi wa mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani ikiwemo Singida na Manyara kwa pamoja wamejadili maboresho ya ufikashaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma na namna ya kushirikiana katika kumpatia Mtanzania huduma bora za afya.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Best Magoma, amesema watahakikisha kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaonekana kwa kutimiza wajibu wao kwa walengwa ambao ni wananchi kufikiwa na huduma bora za afya.