Mradi wa ujenzi wa wodi watiliwa shaka

0
102

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu Luteni Josephine Mwambashi amekataa kuweka jiwe la msingi, ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Luteni Mwambashi amesema nyaraka za ujenzi wa wodi hizo hazijakaa sawa kutokana na kuwepo kwa upotevu wa fedha.

Mradi huo ambao taarifa inaonesha umetumia shilingi milioni 411, huku kwenye nyaraka zilizokaguliwa na Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu inaonesha umetumia shilingi milioni 400, na hivyo kuwepo kwa upotevu wa shilingi milioni 11.

Luteni Mwambashi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini ( TAKUKURU), kuanza kuchunguza ujenzi wa mradi huo ambao ametumia takribani saa mbili kuchunguza nyaraka zake.

Ujenzi huo wa wodi tatu katika hospitali ya wilaya ya Masasi ulianza mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu, na hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 500.