Mradi wa uboreshaji bandari ya Dar es salaam waendelea vizuri

0
2418

Mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es salaam umefikia asimilia 42 ya ujenzi wake hadi hivi sasa huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020.
Hayo yamebainika wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea mradi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mradi huo ambao umelenga kuifanya Bandari ya Dar es salaam kuwa ya kisasa zaidi na kuongeza uwezo wake wa kuhudumia meli kubwa kwa wakati mmoja, unahusisha ujenzi wa gati maalum ya kushushia magari, gati namba moja mpaka namba saba, kuongeza kina cha maji katika magati hayo pamoja na kutanua lango la kuingia meli bandarini.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu ambao hadi sasa umefikia asilimia 42, matarajio yetu mradi huu utaisha kwa wakati uliopangwa,” amesema Mhandisi Nditiye.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) Mhandisi Karim Mattaka amesema kuwa mradi huo wa uboreshaji wa bandari ya Dar es salaam, bado upo ndani ya wakati pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza wakati wa ujenzi wake.
Mhandisi Mattaka amesema kuwa kulikuwa na changamoto kadhaa wakati wa zoezi la kuhamisha mchanga ambapo ilibainika kuwa kuna mchanga laini upo kwenye eneo litakalojengwa gati ya kushushia magari, na hivyo kulazimika kuendelea na ujenzi wa gati namba moja wakati zoezi la kutibu mchanga huo laini likiendelea.
“Ujenzi wa gati namba moja umefikia pazuri kwani unatarajiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Disemba mwaka huu na hivyo kuanza kutumika rasmi kabla ya kuhamia gati namba mbili ,” amesema Mhandisi Mattaka.
Ujenzi wa gati maalum ya kushushia magari unatarajiwa kuanza mara zoezi la kutibu mchanga laini litakapokamilika.