Mradi wa SEQUIP kuboresha elimu

0
479

Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya elimu kwa kuwekeza na kufanya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwenye shule na vyuo, huku ikiwajengea Walimu uwezo wa kiutendaji kupitia mafunzo yanayoendelea kutolewa kupitia mradi wa kuimarisha Shule Salama za Sekondari (SEQUIP).

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia @wizara_elimutanzania Juma Kipanga ameyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi mafunzo na kuzungumza na walimu waliohudhuria mafunzo ya mradi wa SEQUIP yaliyofanyika katika Manispaa ya Lindi.

Amesema katika kutimiza azma ya kuboresha sekta ya elimu nchini, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatekeleza mradi wa SEQUIP kwa thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 500 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 1.2 kwa kipindi cha miaka mitano.

Tangu kuanza kwa mradi huo mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imejenga shule mpya za sekondari 460 na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu pamoja na kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa zaidi ya walimu 25,228 wa sayansi, wadhibiri ubora wa shule 194, maafisa elimu wa mikoa wanane, wahamashauri 58 pamoja na walimu wa somo la TEHAMA katika shule za sekondari 500.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema mradi wa SEQUIP umekuwa na manufaa kwa mkoa wa Lindi kwani katika utekelezaji wa mradi huo mkoa wa Lindi ulikuwa wa kwanza kuwa na shule maalumu ya Wasichana iliyotokana na mradi wa SEQUIP.