Mradi wa Maji Songea kukamilika ndani ya siku 60

0
273

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Litisha katika Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua na kujionea maendeleo ya mradi huo.

“Nimefurahi kuona kisima kinatoa maji mengi sana na tenki tayari limekamilika lakini, bado miundombinu ya kuwafikishia wananchi maji haijakamilika; maelekezo yangu ni kuwa, ndani ya siku 60 mradi huu uwe umekamilika na wananchi wawe wamepata huduma ya maji,” amesema Sanga.

Pia, amewahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali haitowaangusha, itahakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi mapema iwezekanavyo kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Sanga amewataka wananchi kuwa na imani kwa Serikali waliyoichagua kwani kero zao mbalimbali ikiwemo ya maji zitatatuliwa

Mpaka sasa ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji umeanza katika vijiji vinne ambavyo ni Litisha, Litowa, Nakahuga na Peramiho B kwa gharama ya shilingi bilioni 2.4